Sababu za wengi kuchelewa matibabu ya Saratani ya Matiti

Saratani ya matiti, wengine huita Kansa ya matiti ndiyo saratani ya inayoongoza ulimwenguni kote na ndio sababu kuu ya vifo vingi vinavyousiana na saratani kwa wanawake. Idadi ya wanawake wenye saratani ya matiti ni ya juu katika nchi zilizoendelea kuliko nchi za kipato cha chini na kati (Uchumi wa kati). Lakini hata hivyo, kuna uwiano wa juu wa vifo katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati kwa sababu ya wengi kuchelewa kugundulika/kuthibitika kuwa saratani ya matiti au wengi kuchelewa kuanza matibabu sahihi ya saratani. Inakadiliwa wengi huchukua zaidi ya miezi, ambao zaidi ya 70% ya wagonjwa waligundulika wakati saratani imeshasambaa sehemu mbalimbali za mwili kamavile kichwani kwenye ubongo, kwenye mifupa , kwenye mapafu na kwenye ini.

Wamama wengi huja Hospitali kuanza matibabu ya saratani wakiwa wamechelewa, unakuta saratani imeshasambaa tayari. Wengi huja wakiwa na dalili hizi, kushindwa kupumua vizuri, Uchovu, Kushindwa kulala, Tumbo kuvimba, Maumivu ya kifua na nk. Sababu zinazofawanya wachelewe ni hizi hapa chini:

Ucheleweshaji wa kuanza matibabu kwa takriban nusu (48%) ya wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Hospitali za Rufaa ikiwemo Muhimbili na Ocean Road walikuwa wakijihusisha kwa muda mrefu zaidi na uponyaji wa kiroho, wengine hutumia virutubisho vya chakula (Chai/Juice ya majani ya mstaferi/tunda lake) na dawa za mitishamba (dawa za asili). Kunaambao hutumia tiba mbadala hata baada ya kuthibitika Hospitalini kuwa na saratani ya matiti, hii inatokana na imani za kidini, desturi za watu wetu, tamaduni na uelewa wao wa saratani kama “shambulio la kiroho”. Hii hupunguza kwa kiasi kikubwa uanzishwaji wa dawa (chemotherapy) kwa wagonjwa na hata uwezekano wa kufanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe katika hatua za awali za ugonjwa.

Robo ya wagonjwa (24%) walichelewesha matibabu kwa sababu za kifedha. Gharama kubwa ya upasuaji au dawa za kutibu saratani ni changamoto kubwa. Juhudi za Serikali katika kutoa ruzuku ya matibabu na kushirikisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na wahisani katika kuhudumia wagonjwa wa saratani zinaweza kupunguza mzigo wa kifedha kwa wagonjwa.

Hofu ya upasuaji wa matiti hasa upasuaji wa kuondolewa titi lenye saratani ni sababu kuu ya kutoroka matibabu baada ya kuthibitika kuwa na saraani ya titi. Hii ni kwa sababu ya imani potofu ya watu kwamba upasuaji wa kuondolewa titi (mastectomy) mara nyingi husababisha kifo baada ya upasuaji. Tafiti zinaonyesha kuwa 10% ya wagonjwa huchelewa kuanza matibabu kwa sababu ya kuogopa upasuaji wa kuondolewa titi. Kwa kuwa upasuaji wa kuondolewa titi ni sehemu muhimu ya udhibiti wa saratani ya matiti, hasa katika ulimwengu unaoendelea, jitihada zinapaswa kufanywa ili kukabiliana na hofu inayohusishwa na kutoa ushauri wa kutosha, kuruhusu wagonjwa kueleza hofu zao, na kuondoa dhana potofu inayohusisha upasuaji na vifo. kugundulika mapema kwa wagonjwa wapya wa saratani kunaweza kupunguza hofu hii kwani kwenye hatua za awali za ugonjwa hakuitajiki upasuaji wa kuondolewa titi.

Chemotherapy ama kemo ni dawa zinzotumiwa kutibu saratani kwa kuua seli za saratani, kuzuia saratani isisambae au kupunguza uvimbe wa saratani, inakuwa katika hali ya kimiminika au kidonge na kutolewa kwa kunjywa au sindano (dripu). Wagonjwa wengine pia walihusisha hofu ya kemo dhidi ya athari zake kuhisiwa “zinasababisha kifo”. Mtoa huduma ana jukumu kubwa la kutekeleza katika kuhakikisha kuwa wagonjwa wanashauriwa vizuri. Ingawa inaweza kuwa haifai kutafuna maneno katika kuelezea athari za dawa, inaweza kuwahakikishia wagonjwa kuwa athari zake ni za muda na mara nyingi zinaweza kubadilishwa.

Huu ni ule muda mgonjwa ameanza kugundulika kuwa na viashilia vya saratani hadi kuanza matibabu ndani ya kituo cha matibabu. Na hapa kumegawanyika makundi mawili nayo ni:

Hapa muda uliotumika kwa mtoa huduma wa kwanza (toka mgonjwa anakutana na Daktari wa kwanza) kwenye Hospitali ndogo au vituo vya Afya hadi pale anapopatiwa Rufaa. Kimsingi mwanamke mwenye viashilia vya saratani ya titi anatakiwa mapema kuanza kufanyiwa vipimo vya saratani katika Hospitali za Rufaa ilikubaini kama uvimbe huo ni saratani au la.

Katika Hospitali za Rufaa kuna kufanya uchunguzi na vipimo kutibiti uwepo wa saratani ya matiti, lakini kutokana na sababu za mgonjwa mwenyewe mfano sababu za kifedha au Hofu ya matibabu zinaweza pelekea ucheleweshaji wa muda toka mgonjwa apate Rufaa hadi kuanza kwa matibabu.

Kulingana na uainishaji uliotajwa hapo juu, ucheleweshaji wa kuanza matibabu ya saratani baada ya kuthibitika saratani mara nyingi hulaumiwa Hospitali au mfumo wa utoaji huduma na mtoa huduma, kuwaondoa wagonjwa, bila kujali ripoti zinazoonyesha sababu zinazohusiana na mgonjwa mwenyewe tulizozianisha hapo juu ndio sababu kubwa kusababisha ucheleweshaji wa utambuzi na matibabu ya saratani matiti kwa wanawake.

Kuchelewa kwa matibabu ya saratani kwa wagonjwa wenye saratani ya matiti hupunguza umri wa kuishi zaidi ya miaka 5 hata baada ya matibabu. Inakadiliwa ni asilimia 27 hadi asilimia 30 ya wagonjwa wenye saratani ya matiti walioanza matibabu katika hatua ya juu (stage 4) ndio wanaweza kuisha zaidi ya miaka 5 baada ya matibabu. Inatakiwa angalau ndani ya miezi 10 baada ya kua na viashilia vya saratani hadi itakapothibitika kua ni saratani ya matiti mgonjwa awe ameanza matibabu, japo kuanza kwa matibabu ndani ya siku 45 za kwanza baada ya kugunduliwa kwa saratani ya matiti kwa wanawake huongeza Umri wa kuishi na kumfanya aweze kuendelea na kazi zake hata baada ya matibabu, ilhali kucheleweshwa kunapunguza umri wa kuishi na wengi kushindwa kuendelea kufaya kazi zao za kawaida hata baada ya matibabu kutokana na athari ya kusambaa kwa saratani kwenye mifupa na mapafu kumfanya awe mchovu muda wote, wengine kushindwa kutembea na kuvimba sehemu za mwili kama vile tumbo, mkono uliokaribu na titi lililoathirika. Hivyo basi kuchelewa kunaweza kusababisha matokeo mabaya zaidi.

0 0 votes
Article Rating
Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x